morrison-pic

Simba walikuwa na hamu kubwa ya kutaka kuona winga Bernard Morrison anaenda Sauzi kukinukisha kwenye mechi ya marudiano ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates, lakini mambo yametibuka.

Wasauzi wamemkomalia winga huyo raia wa Ghana na kumzuia kutimba huko, licha ya mabosi wa Simba kupambana kwa karibu wiki nzima ili kuweka mambo sawa baada ya kubaini alikuwa na marufuku ya Idara ya Uhamiaji kuingia nchini humo.

Simba imepanga kuondoka kati Aprili 21 au 22 kwenda Sauzi kurudiana na Orlando katika mechi itakayopigwa Aprili 24, lakini Morrison hatakuwa kwenye msafara huo baada ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez kukiri wamekwama.

Barbara alisema rasmi jambo hilo limeshindikana kama ilivyokuwa msimu uliopita walipoenda kucheza na Kaizer Chiefs katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika naa kufungwa mabao 4-0.

Mtendaji huyo alisema taarifa za Morrison na ataenda huko sio za kweli.

“Tuliwasiliana na watu wa Mamlaka za Uhamiaji Afrika Kusini kuomba kupata ruhusa ya kuingia na Morrison, walitueleza sheria zao mtu akivunja hawezi kupata tena nafasi ya kuingia,” alisema Barbara

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *