
Taarifa iliyotumwa na timu ya Uber kwa wateja wake nchini imeweka wazi kuwa wameamua kusitisha huduma zake nchini kuanzia leo, Aprili 14, 2022.
Taarifa imetumwa kwenye email za wateja jana Jumatano Aprili 13, 2022 imesema kuwa huduma za UberX, UberXL na UberX Saver hazitapatikana nchini Tanzania.
Sababu zilizotajwa za kusitisha huduma hiyo ni kutokana na kanuni za usimamizi wa sekta hiyo kujenga mazingira ambayo si rafiki na zimekuwa changamoto kubwa katika uendeshaji wa biashara hiyo.
“Tumechukua uamuzi mgumu wa kusitisha kwa muda huduma za UberX, UberXL na UberX Saver nchini Tanzania, bidhaa hizi hazitapatikana kuanzia Alhamis 14 Aprili 2022. Kanuni za sasa za usimamizi wa sekta hii zimejenga mazingira ambayo si rafiki na zimekuwa changamoto kubwa katika uendeshaji wa biashara yetu, hadi pale muafaka utakapopatikana, hatutaendelea kutoa huduma za usafiri wa UberX, UberX Saver na UberXL nchini Tanzania.
“Huu ni wakati mgumu kwetu sote, lakini hii haina maana kwamba ndio mwisho wa kila kitu.
“Tuko tayari kushirikiana na mamlaka husika na kuwa na mazungumzo yatakayoleta tija na kujenga mazingira wezeshi na tutarudi na kuendelea na kukupa usafiri wa kutegemewa na wa uhakika ambao umekuwa ukiitumia, baada ya kujiridhisha kwamba mazingira ya kibiashara ni rafiki” Taarifa ya Uber.