tetemeko.png

Wengi wa waliofariki na kujeruhiwa katika tetemeko kubwa la ardhi katika kisiwa cha Java nchini Indonesia walikuwa watoto waliokuwa shuleni wakati lilipopiga, waokoaji walisema. Aprizal Mulyadi, 14, alisema alinaswa baada ya “chumba kuporomoka na miguu yangu kufukiwa chini ya vifusi”.

Alisema alivutwa hadi salama na rafiki yake Zulfikar, ambaye baadaye alifariki baada ya yeye mwenyewe kunaswa. Utawala wa eneo la Cianjur unasema idadi ya vifo imeongezeka hadi watu 252. Mapema siku ya Jumanne wakala wa kitaifa wa kukabiliana na majanga nchini Indonesia, BNPB, uliweka vifo vilivyothibitishwa kuwa 103 huku watu 31 wakikosekana – lakini ilionya kwamba idadi hii inaweza kuongezeka.

Tetemeko hilo la kipimo cha 5.6 katika kipimo cha Richter lilipiga eneo la milima siku ya Jumatatu, na kusababisha maporomoko ya ardhi yaliyozika vijiji vyote karibu na mji wa Cianjur Magharibi mwa Java. Waathiriwa walikandamizwa au kunaswa baada ya kuta na paa kuporomoka. “Yote yalitokea haraka sana,” Aprizal aliliambia shirika la habari la AFP. Mwakilishi wa Shirika la Kitaifa la Utafutaji na Uokoaji pia alithibitisha kwamba wengi wa waliokufa walikuwa vijana. “Majeruhi wengi ni watoto kwa sababu saa moja usiku walikuwa bado shuleni,” alisema Henri Alfiandi.

Tetemeko hilo la ardhi lililopiga katika kina kirefu cha kilomita 10, lilifuatiwa na makumi ya mitetemeko ya ardhi iliyosababisha uharibifu zaidi katika eneo ambalo nyumba zilizojengwa vibaya zilianguka haraka. Katika kijiji cha Cibereum, familia ilikuwa ikijaribu kuuchukua mwili wa mtoto wao mkubwa – mwanamume mwenye umri wa miaka 28 ambaye alikuwa amepondwa hadi kufa wakati ngazi nyingine za nyumba hiyo zilipomwangukia.

Waokoaji walijitahidi kupekua vifusi. “Tunalazimika kuchimba saruji ya ghorofa ya pili iliyomponda mwathiriwa. Lakini tumeuona mwili huo,” afisa wa kijeshi, First Sajenti Payakun alisema. Mamlaka inasema angalau nyumba 2,200 zimeboreshwa na zaidi ya watu 13,000 kuhamishwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *