
Mchezo wa ‘Kariakoo Derby’ kati ya Simba na Yanga umemalizika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa wenyeji kushinda mabao 2-0
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi nchini humo ,mabao ya Simba yamefungwa na beki, Henock Inonga dakika ya pili ya mchezo huku Kibu Denis akifunga la pili kwa shuti kali lililomshinda kipa Diarra dakika ya 32.
Huu ni mchezo wa 110 baina ya timu hizi kukutana katika Ligi Kuu Bara tangu mwaka 1965 ambapo kati ya hiyo Yanga imeshinda 38 huku Simba ikishinda 32 na mechi 40 zikiisha kwa sare.
Kulingana na gazeti hilo , katika michezo hiyo 110 safu ya ushambuliaji ya Yanga ndio ambayo imekuwa tishio tofauti na kwa wapinzani wao kwa sababu imefunga jumla ya mabao 113 huku kwa Simba ikifunga 103.
Mabao tisa (9) kati ya 14 yaliyofungwa katika mechi 11 zilizopita za Ligi Kuu Bara baina ya timu hizi yamewekwa kimiani na wachezaji wa kigeni huku matano tu yakifungwa na wazawa.