
Paka mwitu aliyegunduliwa kuwa na cocaine anapona katika Bustani ya Wanyama ya Cincinnati na Bustani ya Mimea, katika jimbo la Ohio, Marekani, baada ya tukio la kiwewe ambalo lilimfanya kujeruhiwa.
Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kwa utani wamemwita “Cocaine Cat” – rejeleo la filamu iliyotolewa hivi majuzi ya Cocaine Bear, iliyochochewa na hadithi ya maisha halisi kuhusu dubu mweusi mwenye uzito wa kilo 80 ambaye anafanya fujo baada ya kumeza cocaine.
Servals (Paka mwitu) ni aina asili ya Afrika, hasa wanaopatikana wakizurura katika nyanda za chini ya jangwa la Sahara na vichaka.
Ni wakubwa na warefu kuliko paka wa kufugwa wanafikia urefu wa hadi 60cm – na wanaweza kukua na kuwa na uzito kati ya kilo 8 na 20k, ambayo kwa kawaida huwa karibu na ukubwa wa mbwa mdogo.

Mapema asubuhi ya tarehe 28 Januari, Huduma za Walezi wa Mbwa wa Kaunti ya Hamilton (kitengo cha Cincinnati Animal CARE) ziliitwa kuchunguza ripoti za “chui” aliyeonekana kwenye mti.
Paka huyo alitoroka huku polisi wa Cincinnati wakimkamata mwanaume mmoja kwenye kituo cha trafiki, kulingana na meneja wa ushiriki wa jamii wa Cincinnati Animal CARE, Ray Anderson. Aliambia BBC kwamba mnyama huyo kwa jina Amiry, aliruka kutoka kwenye gari la mwanaume huyo na kukimbia juu ya mti,
Bw Anderson alisema paka huyo “hakufurahishwa” kuondolewa kwenye mti huo. Alisema maofisa wenzake hawakujua wanakabiliana na nini na kwa mtazamo wangeweza kufanya kazi na timu kubwa kumnasa paka huyo.
“Wazo letu la awali lilikuwa paka huyo alikuwa mseto wa F1 Savannah, ambayo ni halali kumiliki huko Ohio. Lakini mtaalamu wetu alikuwa na hakika kwamba Amiry alikuwa serval, ambayo ni kinyume cha sheria,” Bw Anderson alisema.
Paka F1 Savannah ni aina mchanganyiko wa paka wa nyumbani na wa mwituni.

“Timu yetu ya matibabu ilimchunguza Amiry, na kuchukua sampuli kwa ajili ya kipimo cha DNA na kumfanyia vipimo vya narcotics. Amiry alipimwa na kukutwa na cocaine na kipimo cha DNA kilihitimisha kuwa kweli alikuwa paka mwitu( serval)
Wakati wa misheni ya uokoaji, paka alifadhaika na akavunjika mguu.
Banda la wanyama, ambalo kwa kawaida hutunza wanyama wa kufugwa, halikuwa na vifaa vya kuweka paka-mwitu. Kwa hivyo, alisafirishwa salama hadi Bustani ya Wanyama ya Cincinnati na Bustani ya Mimea kwa matibabu zaidi.
“Tunajivunia sana kazi iliyofanywa katika tukio hili na walinzi wa mbwa na wafanyakazi wa matibabu, na tunathamini sana Bustani ya Wanyama ya Cincinnati kwa kumpatia Amiry utunzaji anaohitaji,” Bw Anderson aliongeza.
Bado haijulikani jinsi paka ilivyomeza kumeza dawa hiyo.

Bw Anderson anasema mmiliki wa paka huyo amekuwa akishirikiana na uchunguzi huo. Udhibiti wa wanyama wa eneo hilo, Huduma ya Walinda Mbwa wa Kaunti ya Hamilton, haitarajiwi kushtaki kwa wakati huu.
Lakini kesi bado iko wazi na Idara ya Kilimo ya Ohio inachunguza.