
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limesema January 23,2024 majira ya Jioni limepokea taarifa ya mtoto wa kiume mwenye umri wa Miaka 3 na miezi 8 kutekwa na mtu mmoja ambaye hakuweza kufahamika jina wakati mtoto huyo alipokuwa akitoka kucheza kwenye nyumba ya jirani katika maeneo ya Mji Mpya, Wilayani Korogwe
Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga Almachius Mchunguzi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ambapo amesema kufuatia tukio hilo uchunguzi ulianza na kubainika mtu huyo asiyefahamika alimtaka mama mzazi wa mtoto huyo atoe kiasi cha Shilingi 1,500,000/= ili aweze kumrejesha mtoto huyo.
Amesema January 25, 2024 majira ya ya Mchana huko katika Kitongoji cha Sagama “A” Kijiji cha Kwamkono Tarafa ya Sindei, Wilaya ya Handeni Askari Polisi waliokuwa wanafuatilia tukio hilo wamefanikiwa kumkamata Ramadhani Adinai Almaarufu kama MBANO (21) Mkazi wa Manundu akiwa na mtoto huyo.
Kamanda Mchunguzi amesema mtoto huyo amepelekwa kwa wataalamu wa Afya kwa Uchunguzi ja Taratibu za Kumrejesha kwa Mama yake zifanyike, ambapo ameongeza kuwa Taratibu za kisheria zikikamilika mtuhumiwa huyo atafikishwa Mahakamani.
Aidha ametoa wito kwa Wazazi na walezi kuendelea kuwalinda watoto wao kwa karibu ili kuwaepusha na Vitendo vya watu wenye nia ovu kama vile Utekaji, kubaka na kulawiti.