
Katibu tawala wa Wilaya ya Kigoma Mganwa Nzota amekemea tabia za Wananchi wanaoharibu miundombinu ya nguzo na vibao vya anwani ya Makazi na kutumia kama vyuma chakavu.
Ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi kwa Watendaji wa Kata, Mitaa na Wenyeviti wa Mitaa katika ukumbi wa Redcross yanayotolewa na Wataalamu kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari.
Mh. Nzota amewataka Watendaji wa Kata, Mitaa na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kushirikiana na Wananchi kuwabaini Waharifu na kuwachukulia hatua katika kuharibu miundombinu ya Postikodi.
Akiwasilisha mada Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Charles Watson Gombo amesema lengo la zoezi hilo ni kusasisha taarifa na miundombinu iliyofanyika kwa kipindi kilichopita, kuhuisha na kukusanya taarifa mpya.
Amesema mafunzo hayo yanatarajia kufanyika kwa muda wa siku mbili na zoezi la uhakiki wa taarifa ukifanyika kwa siku kumi na mbili kwa kushirikisha Viongozi hao na Wananchi katika mitaa sitini na nane 68 ya Manispaa Kigoma Ujiji.
Utambuzi na uwekaji wa Anwani za makazi Nchini ulifanyika na unafanyika kwa kutoa namba ya anwani (namba ya jengo, au kiwanja), majina ya barabara au kitongoji na postikodi.