
Serikali Wilayani Ludewa Mkoani Njombe imepiga marufuku ulaji wa nyama ya Nguruwe, kuingiza mfugo wa Nguruwe pamoja na kutumia mazao yeyote ya Nguruwe ikiwemo Damu, samadi, mifupa na nywele kwa muda usiojulikana isipokuwa kwa idhini ya Daktari wa mifugo wa Wilaya hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Daktari wa mifugo wa Wilaya hiyo Dkt. Festo Mkomba imeeleza yafuatayo “kwa Mamlaka niliyopewa na sheria ya mifugo namba 16 (2),17 ya mwaka 2003, kuanzia leo tarehe 15/03/2023 natangaza kwamba Wilaya ya Ludewa itakuwa chini ya Karantini mpaka hapo itakavyotangazwa vinginevyo hii ni kutokana na matukio ya ugonjwa wa homa ya Nguruwe kujitokeza katika Wilaya ya Ludewa”
Taarifa hiyo imeeleza kuwa adhabu kali itatolewa kwa mujibu wa sheria kwa yeyote atakayekiuka masharti yaliyotolewa kutokana na uwepo wa ugonjwa huo wa homa ya Nguruwe.