
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda na mgombeaji mara mbili wa urais, Nobert Mao ametia saini makubaliano ya ushirikiano na chama tawala cha National Resistance Movement kufuatia mkutano na Rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni katika Ikulu ya Entebbe siku ya Jumatano.
Museveni alituma video fupi ya kutiwa saini kwa makubaliano hayo kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Aliwasifu viongozi wa Chama cha Democratic kwa kile alichotaja kuwa ni ishara ya ukomavu, mtazamo wa mbele na siasa za kujenga.
Mao amekuwa rais wa chama cha Democratic tangu 2010 na alianza kuonekana katika siasa za kitaifa mwaka 1996 alipochaguliwa kuwa mbunge ambapo alihudumu kwa mihula miwili.
Alijitokeza kwa ufasaha wake na msimamo wake wa kupinga
Wakati huo huo Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametetea uamuzi wa serikali yake wa kutotoa ruzuku au kupunguza ushuru akisema pesa hizo zingetumika kutatua shida zinazoikabili nchi.
Alikuwa akihutubia taifa katika hotuba iliyorushwa kwenye televisheni Jumatano usiku huku kukiwa na ongezeko kubwa la kupanda kwa gharama za maisha kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta na uhaba wa chakula katika baadhi ya maeneo nchini.
Rais Museveni alisema ruzuku inawapotosha watu kufikiri kwamba kuna mengi na wanashindwa kujipanga kiuchumi kwa kile walichonacho na hatimaye kumaliza akiba ya kigeni ya nchi.
Alisema kupunguzwa kwa ushuru pia kutasababisha kukwama kwa miradi ya miundombinu.