
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametangaza kufutilia mbali maandamano ya kuipinga serikali kuanzia kesho ili kutoa fursa kwa mazungumzo na upande wa serikali .
Amesema muungano wa Azimio uko tayari kwa mazungumzo kuhusu masuala walioibua endapo serikali iko tayari kufanya majadiliano .

Bw Odinga Aliangazia Mambo yafuatayo:
- Wana haki ya kufanya maandamano. Ikiwa hakuna jibu, watarejelea maandamano baada ya wiki moja
- Wanasisitiza kwamba maandamano ni haki ya kimsingi iliyoainishwa katika katiba ya Kenya
- Azimio kukumbatia mazungumzo na kushirikisha timu ya Dkt Ruto kwa suluhu la amani kwa matatizo yanayokumba nchi.
- Azimio inataka makamishana wanne (Cherera 4 )warejeshwe kazini
- Azimio iko tayari kwa mchakato wa mazungumzo kuanzia kesho
- Kushughulikia gharama ya juu ya maisha Ni sharti mojawapo lisiloweza kuondolewa kwenye orodha ya matakwa yao.
- Serikali inapaswa kurudi kwenye mpango wa ruzuku uliotumiwa na serikali ya zamani
Awali rais William Ruto aliutaka upinzani kufutilia mbali maandamano hayo
Rais wa Kenya William Ruto amemtaka kiongozi wa upinzani Raila Odinga kusitisha maandamano ya kesho na kukubaliana na mojawapo ya matakwa ya Bw Odinga ushirikiano wa pande mbili bungeni kuhusu kuundwa kwa tume mpya ya uchaguzi, IEBC.
Nafasi zote saba za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ziko wazi. Bw Odinga amepinga jopo la sasa la uteuzi .
Lakini rais amependekeza kuwa hatamshirikisha Raila kuhusu matakwa yake mengine, ikiwa ni pamoja na gharama ya juu ya maisha na uhalali wa urais wake.
Tume ya uchaguzi nchini Kenya ilimtangaza Ruto kuwa mshindi mwaka jana, na mahakama ya juu zaidi ikakubali ushindi wake. Lakini Bw Odinga anasisitiza kuwa alishinda uchaguzi huo.
Siku ya Jumamosi alichapisha matokeo yake mbadala kupitia tovuti huru na anadai kufunguliwa kwa seva za uchaguzi wa urais ili kuthibitisha ni matokeo gani ni sahihi.
Takriban Wakenya 3, miongoni mwao afisa mmoja wa polisi wameuawa tangu maandamano ya kwanza tarehe 20 Machi.