Ripoti iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu imekosoa vikali jinsi Shirika la Ujasusi la Marekani (FBI) inavyoshughulikia uchunguzi wake kuhusu madai ya uhusiano kati ya Urusi na kampeni ya Trump ya 2016.
Katika ripoti ya kurasa 306, wakili maalum John Durham alisema uchunguzi wa shirika hilo haukuwa na “makali ya uchambuzi”.
Alihitimisha FBI haikuwa na “ushahidi halisi” wa ushirikiano kati ya kampeni ya Donald Trump na Urusi kabla ya kuanzisha uchunguzi.
FBI ilisema imeshughulikia masuala yaliyoangaziwa kwenye ripoti hiyo.
Katika ripoti hiyo, Bw Durham – ambaye aliteuliwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa wakati huo William Barr mnamo 2019 – alishutumu FBI kwa kuchukua hatua kwa “taarifa ambazo hazijakamilika kuchunguzwa kijasusi”.
Miongoni mwa makosa ya kiuchunguzi iliyofanya ni matukio ya mara kwa mara ya “upendeleo wa uthibitisho”, ambapo ilipuuza habari ambayo ilipunguza msingi wa awali wa uchunguzi.
Ripoti hiyo ilibainisha tofauti kubwa katika jinsi FBI walivyoshughulikia uchunguzi wa Trump ikilinganishwa na maswali mengine yanayoweza kuwa nyeti, kama yale yaliyomhusisha mpinzani wake Hillary Clinton katika uchaguzi wa 2016.
Bw Durham alibainisha kuwa Bi Clinton na wengine walikuwa wamepokea “maelezo kidogo ya kujihami” kutoka kwa FBI yaliyolenga “wale ambao wanaweza kuwa walengwa wa shughuli chafu na mataifa ya kigeni”. Bw Trump hakufanyiwa hivyo.
“Idara [ya Haki] na FBI zilishindwa kuendeleza dhamira yao muhimu ya uaminifu mkubwa kwa sheria,” ripoti hiyo ilihitimisha.
Katika taarifa, FBI ilisema “tayari imetekeleza makumi ya hatua za kurekebisha hilo”.
“Kama mageuzi hayo yangefanyika mwaka wa 2016, makosa yaliyoainishwa kwenye ripoti yangezuiwa,” imeongeza taarifa hiyo.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Uchunguzi wa FBI kuhusu madai ya uhusiano kati ya kampeni ya Trump na Urusi, ambao ulifanywa na Wakili Maalum Robert Mueller, ulisababisha mashtaka kadhaa ya jinai dhidi ya wafanyikazi wa kampeni ya Trump na washirika wake kwa uhalifu ikiwa ni pamoja na udukuzi wa kompyuta na uhalifu wa kifedha.
Hata hivyo, haikugundua kuwa kampeni ya Trump na Urusi walikuwa na njama pamoja kushawishi uchaguzi.
Akiandika kwenye mtandao wake wa kijamii, Truth Social, Bw Trump alisema ripoti ya Durham ilionyesha kuwa “raia wa Marekani walilaghaiwa”.
Alitoa mfano wa hitimisho la ripoti hiyo kuwa hakujakuwa na ushahidi wa kutosha kuwezesha uchunguzi kamili wa FBI.
Bw Trump amedai kwa muda mrefu kuwa wanachama wa “serikali” wanamlenga isivyo haki.
Mwaka jana, Bw Trump alisema anaamini kwamba ripoti ya Durham itatoa ushahidi wa shughuli “mbaya, uovu na kinyume cha sheria” na “kufichua ufisadi kwa kiwango ambacho hakijawahi kuonekana nchini mwetu”.
Ripoti ya Durham ina mapungufu ya ufichuzi wenye uzito na mashtaka ambayo washirika wengine wa Trump walitarajia yangechipuka kutoka kwa uchunguzi huo.
Badala yake, matokeo ya uchunguzi huo wa miaka minne yamekuwa ni mashtaka matatu ambayo ni pamoja na wakili wa FBI ambaye alikiri makosa ya kubadilisha ushahidi wakati akiomba ruhusa ya kumsikiliza afisa wa zamani wa kampeni ya Trump.
Watu wengine wawili waliachiliwa kwa tuhuma za kudanganya FBI.
Rais huyo wa zamani alitaja baadhi ya kesi zilizowasilishwa mahakamani na timu ya Durham kuwa ni sehemu ya kesi aliyowasilisha dhidi ya Bi Clinton na maafisa wengine kadhaa wa chama cha Democrat na serikali, kwa madai kwamba walikuwa na njama ya kudhoofisha azma yake ya kugombea urais 2016 kwa kueneza uvumi kuhusu uhusiano wa kampeni yake na Urusi.
Jaji alitupilia mbali kesi hiyo akisema ni ya kipuuzi mnamo Januari na kuamuru Bw Trump alipe takriban dola milioni moja kama adhabu.
Bw Durham na uchunguzi wake kuna uwezekano wakaendelea kugonga vichwa vya habari vya kitaifa katika siku za usoni.
Muda mfupi baada ya habari kwamba ripoti hiyo itatolewa hadharani, Mwenyekiti wa Kamati ya Mahakama ya Bunge Jim Jordan alitangaza kuwa atampigia simu mwanasheria huyo wa zamani wa Marekani kutoa ushahidi mbele ya Bunge la Congress kuhusu kazi yake.