
Kundi la Taliban limepiga marufuku wanawake kutoka vyuo vikuu nchini Afghanistan, na hivyo kuzua lawama za kimataifa na kukata tamaa miongoni mwa vijana nchini humo.
Waziri wa elimu ya juu alitoa tangazo hilo siku ya Jumanne, akisema litaanza kutekelezwa mara moja.
Marufuku hiyo inazuia zaidi elimu ya wanawake – wasichana tayari wametengwa kutoka shule za upili tangu Taliban iliporejea mwaka jana.
Huko Kabul, wanafunzi wa kike wamezungumza kuhusu uchungu wao. “Waliharibu daraja pekee ambalo lingeweza kuniunganisha na maisha yangu ya baadaye,” mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Kabul alisema. “Ninawezaje kuitikia? Niliamini kwamba ningeweza kusoma na kubadili maisha yangu ya baadaye au kuleta mwanga kwenye maisha yangu lakini waliiharibu.” Marekani siku ya Jumanne ililaani vikali vitendo vya Taliban “kwa maneno makali” na kusema hatua kama hiyo “itakuja na matokeo kwa Taliban”. “Taliban haiwezi kutarajia kuwa mwanachama halali wa jumuiya ya kimataifa hadi waheshimu haki za wote nchini Afghanistan,” Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken alisema katika taarifa yake.
“Hakuna nchi inayoweza kustawi wakati nusu ya wakazi wake wamezuiliwa.” Nchi za Magharibi zimedai mwaka mzima kwamba Taliban kuboresha elimu ya wanawake ikiwa wanataka kutambuliwa rasmi kama serikali ya Afghanistan. Umoja wa Mataifa pia ulisema “una wasiwasi mkubwa”. “Elimu ni haki ya kimsingi ya binadamu.
Mlango uliofungwa kwa elimu ya wanawake ni mlango uliofungwa kwa mustakabali wa Afghanistan,” alisema Ramiz Alakbarov, naibu mwakilishi maalum wa mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan. Kiongozi wa Taliban Hibatullah Akhundzada na watu wake wa ndani wamekuwa wakipinga elimu ya kisasa – hasa kwa wasichana na wanawake.
Kundi la Taliban lilikuwa limeahidi sheria nyepesi baada ya kutwaa mamlaka mwaka jana kufuatia Marekani kujiondoa nchini humo. Hata hivyo Waislam wenye msimamo mkali wameendelea kurudisha nyuma haki na uhuru wa wanawake nchini humo.
Marufuku ya elimu ya juu inafuata sheria zilizowekwa mwezi uliopita, ambapo wanawake walipigwa marufuku kutoka kwa mbuga, ukumbi wa michezo na bafu za umma katika mji mkuu.