
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewafutia kesi wafanyabiashara wanne waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka 16 yakiwemo ya kula njama na kughushi stika za dawa zilizokwisha muda wake, kwa kuziongezea muda wa matumizi, baada ya kesi hiyo kushindwa kuendelea kwa muda mrefu.
Kesi hiyo iliyokuwa katika hatua ya usikilizwaji wa shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, imefutwa baada ya upande wa utetezi kuwasilisha ombi mahakamani hapo la kuifuta kesi hiyo kutokana na kutoendelea mara kwa mara.
Hata hivyo muda mfupi baada ya kuachiwa huru, washtakiwa hao walikamatwa tena na kuzua tafrani mahakamani hapo baina ya wakili wa utetezi dhidi ya askari Polisi walikuwa wanataka kuwakamata washtakiwa hao.
Washtakiwa hao walikuwa wanakabikiwa na kesi ya jinai namba 99 ya mwaka 2019 yenye mashtaka 16, ambapo mashtaka 15 kati ya hayo; ni ya kughushi stika za dawa zilizoisha muda wake na shtaka moja ni la kula njama ya kutenda makosa ya kughushi.
Waliofutiwa kesi hiyo ni Khalid Somoe (54) mkazi wa Keko Mwanga; Raphael Lyimo (40), mkazi wa Kimara Bonyokwa; Betty Mwakikusye(41) mkazi wa Chanika Msumbiji na Abdiel Mshana(57) mkazi wa Msasani Ubalozini, wote ni wakiwa ni wafanyabiashara.(Kwa mujibu wa ripoti ya Mwananchi)