
Serikali ya Tanzania imesema ushoga, usagaji na ndoa za jinsia moja hazina nafasi Tanzania na kusisitiza kuwa huo ndio msimamo wa Serikali, msimamo wa Rais wa Tanzania Dkt. Samia na Wasaidizi wake.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye @napennauye ametoa msimamo huo usiku wa kuamkia leo wakati akifungua Tamasha la Pasaka lililofanyika katika viwanja vya Leaders Club, Dar es salaam.
“Rais Samia na Serikali ya awamu ya sita tumewasikieni Viongozi wa Dini mkisema waziwazi mnataka Taifa letu lisimamie nini kwenye maadili na utamaduni wetu, tumewaeleweni na ndio msimamo wa Serikali ya Rais Samia, Nchi yetu haitopelekwa kwenye utamaduni wa kigeni” —— amesema Waziri Nape.
“Vitabu vyote vya Dini ikiwemo Katiba yetu ipo wazi juu ya haya ambayo Viongozi wa Dini mmeyakemea, kwa niaba ya Serikali nataka niwahakikishieni Watanzania, ushoga, usagaji, mapenzi ya jinsia moja hayana nafasi Tanzania”
“Wala hakuna sababu ya kumung’unya maneno, msimamo wetu upo wazi Mungu amelibariki Taifa hili hatuwezi kufungua mlango wa laana, salamu za Rais yupo na Viongozi wa Dini wa Nchi hii, mmeonesha ujasiri waziwazi kuyakemea haya, Rais anawaungeni mkono na sisi Wasaidizi wake tunawaungeni mkono ili Taifa letu liendelee kuwa na Baraka”