Capture
Puto ya China iliyoruka juu ya anga ya Marekani mapema mwaka huu ilifanikiwa kukusanya taarifa za kijasusi kutoka kambi za kijeshi kwa siku kadhaa kabla ya kuangushwa, vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti.

Puto hiyo iliweza kutuma data hadi Beijing kwa wakati halisi, kwa mujibu wa NBC News, ikinukuu maafisa wa Marekani.

Kifaa hicho kilikusanya mawimbi ya kielektroniki badala ya kupiga picha, kulingana na afisa mmoja aliyenukuliwa na NBC.

Ikulu ya White House haikuthibitisha ripoti hiyo.

Lakini maafisa wa Marekani wanasema waliweza kupunguza uwezo wa kukusanya taarifa za kijasusi za puto hiyo ilipoelea kote nchini.

Siku ya Jumatatu, msemaji wa idara ya ulinzi alisema kuwa FBI bado ilikuwa inachunguza vifusi vya puto hiyo.

“Tunajua kwamba puto iliweza kuongozwa na kuendeshwa kimakusudi kwenye njia yake,” alisema msemaji Sabrina Singh, ambaye alikataa kusema ni maeneo gani ya kijeshi ambayo puto hiyo iliweza kupita.

“Bado tunafanya tathmini ya taarifa iliweza China iliweza kukusanya lakini tunajua kuwa hatua tulizochukua zilitoa thamani ndogo kwa kile ambacho wameweza kukusanya kutoka kwa satelaiti hapo awali,” alisema.

Puto iliruka wapi?

Maafisa wa Marekani wanasema walifuatilia puto hiyo juu ya Alaska na Kanada kabla ya kuingia tena kwenye anga ya Marekani mapema Februari.

Puto hiyo – iliyokuwa na urefu wa takriban mita 60 – ilidunguliwa katika pwani ya South Carolina tarehe 4 Februari na ndege ya kivita ya Marekani.

Maafisa wa Marekani baadaye walisema walikuwa wameipata puto hiyo. Maafisa wa China wanasema kuwa ilikuwa ni puto ya kiraia ya kuchunguza hali ya hewa na kwamba Marekani ilijibu kwa ukali kwa kuiangusha.

Maafisa waliviambia vyombo vya habari vya Marekani kwamba China iliweza kudhibiti puto hiyo ili iweze kupita mara kadhaa juu ya kambi za kijeshi.

Tukio hilo lilizua mzozo wa kidiplomasia na kusababisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinked kusitisha safari ya China.

Wiki chache baada ya puto hilo kudunguliwa, ndege za kivita za Marekani ziliangusha puto zingine kadhaa ambazo walishuku kuwa zilitoka China. Idara ya ulinzi ya Marekani inasema China inaendesha puto kadhaa duniani kote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *