
Kambi ya Umoja wa Mataifa imelipuliwa kwa bomu la petroli huko Beni, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku kukiwa na maandamano yanayozidi kuwa mabaya dhidi ya Umoja wa Mataifa.
Takribani vituo vingine viwili vya kulinda amani vilishambuliwa pia siku ya Alhamisi.
Takwimu za majeruhi hazikufahamika mara moja. Takriban watu 19 wakiwemo walinda amani watatu wa Umoja wa Mataifa wamefariki katika mapigano hayo makali kufuatia maandamano ya kupinga Umoja wa Mataifa yaliyoanza Jumatatu.
Waandamanaji wamekuwa wakishutumu Umoja wa Mataifa kwa kutowalinda raia dhidi ya makundi yenye silaha yanayoendesha shughuli zake mashariki mwa nchi.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa anasema waandamanaji hao wameunganishwa na vikundi vya wanamgambo wa Mai Mai, vilivyoundwa kwa namna ya kuwalinda wanakijiji.
Zaidi ya makundi 100 tofauti yenye silaha yanaendesha harakati zake mashariki, ikiwa ni pamoja na Allied Democratic Front ambayo inashirikiana na kundi la Islamic State.
Wimbi la hivi majuzi la mashambulizi limeua mamia na maelfu ya wengine kuyahama makazi yao.