
Maelfu ya watu wamejitolea kuasili mtoto wa kike aliyezaliwa chini ya vifusi vya jengo lililoporomoka kaskazini-magharibi mwa Syria, kufuatia tetemeko la ardhi la Jumatatu. Alipookolewa, mtoto Aya – maana yake muujiza kwa Kiarabu – alikuwa bado ameunganishwa na mamake kwa kitovu chake.
Mama yake, baba yake na ndugu zake wote wanne walifariki baada ya tetemeko hilo kupiga mji wa Jindayris. Aya sasa yuko hospitali. “Alifika Jumatatu akiwa katika hali mbaya sana, alikuwa na matuta, michubuko, alikuwa baridi na anapumua kwa shida,” alisema Hani Marouf, daktari wa watoto akimtunza.
Sasa yuko katika hali thabiti. Video za uokoaji wa Aya zilienea kwenye mitandao ya kijamii. Picha zilionyesha mwanamume akikimbia kutoka kwa uchafu wa jengo lililoporomoka, akiwa amemshikilia mtoto mchanga aliyefunikwa na vumbi. Khalil al-Suwadi, jamaa wa mbali, ambaye alikuwepo wakati alipotolewa mahali salama, alimleta mtoto mchanga kwa Dk Marouf katika jiji la Syria la Afrin.
Maelfu ya watu kwenye mitandao ya kijamii sasa wameomba maelezo ya kumuasili. “Ningependa kumchukua na kumpa maisha ya heshima,” alisema mtu mmoja. Mtangazaji wa televisheni ya Kuwait alisema, “Niko tayari kumtunza na kumlea mtoto huyu… ikiwa taratibu za kisheria zitaniruhusu.”
Meneja wa hospitali, Khalid Attiah, anasema amepokea simu nyingi kutoka kwa watu kote ulimwenguni wakitaka kuasili mtoto Aya. Dk Attiah, ambaye ana binti aliyemzidi umri wa miezi minne tu, alisema, “Sitaruhusu mtu yeyote kumlea kwa sasa.
Hadi familia yake ya mbali itakaporudi, ninamchukulia kama mmoja wangu.” Kwa sasa, mkewe anamnyonyesha pamoja na binti yao wenyewe. Katika mji wa nyumbani kwa Aya wa Jindayris, watu wamekuwa wakitafuta wapendwa wao katika majengo yaliyoporomoka.