
Serikali ya Tanzania imetuma helikopta mbili nchini Malawi sambamba na kutoa dola milioni moja taslimu kwa ajili ya kusaidia walioathiriwa wa kimbunga Freddy.
Pia imetoa chakula tani 1,000, mablanketi 6,000 na mahema 50 kwaajili ya kusaidia wahanga nchini humo.
Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Gaudentius Ilonda amesema, “Helikopta mbili zimeruka kutoka Dar es salaam kwenda Malawi kwaajili ya kusaidia katika shughuli mbalimbali za uokoaji katika maafa yanayoendelea.
“Pia serikali imetoa vifaa mbalimbali kama blanketi na mahema… sambamba na shehena za chakula zitapelekwa kila siku nchini Tanzania mpaka kufukia tani 1000,” amesema.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Humphrey Polepole amethibitisha msaada huo kwa Malawi na kuongeza kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kusaidia nchi hiyo katika kipindi hichi kigumu.
“Katika kuhakikisha ndugu zetu wa Malawi wako salama na kuvuka kipindi hiki vizuri. Serikali ya Tanzania imetoa msaada ukiwemo wa fedha taslimu dola milioni moja, chakula, helikopta na vifaa vingine, ” alisema Polepole.
Tanzania inapakana na Malawi na imekuwa na mwingiliano mkubwa wa watu kutoka kwenye mataifa yote mawili.(BBC Swahili)