
Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema anatoa “kipaumbele” kwa uhusiano na nchi za Afrika huku akitafuta washirika wa kimataifa katika kukabiliana na vikwazo vya Magharibi kutokana na uvamizi wa Ukraine.
“Nataka kusisitiza kwamba nchi yetu daima imekuwa ikitoa na itaendelea kutoa kipaumbele kwa ushirikiano na mataifa ya Afrika,” Bw Putin alisema Jumatatu katika mkutano kuhusu uhusiano wa Urusi na Afrika mjini Moscow.
Alisema Urusi itasambaza vyakula kwa nchi zenye uhitaji barani Afrika bila malipo ikiwa makubaliano ya mauzo ya nafaka ya Ukraine hayatafanywa upya.
“Tuko tayari kusambaza kiasi kilichotumwa zamani kwa nchi za Afrika hasa zinazohitaji kutoka Urusi bila malipo kwa nchi hizi,” alisema, kulingana na shirika la habari la Urusi Tass.
Alisema Urusi itashiriki teknolojia yake na mataifa ya Afrika na kuendelea kuyasaidia kuzalisha umeme.
Urusi imekuwa ikipanua ushawishi wake barani Afrika katika miaka ya hivi majuzi na Bw Putin alisema anaamini hilo litaendeleza mamlaka na jukumu lake katika “ulimwengu ambao nguvu yake inazidi kuendea kwanchi nyingi”.
Mkutano huo unahudhuriwa na zaidi ya wajumbe 40 kutoka nchi za Afrika, kulingana na huduma ya vyombo vya habari vya Kremlin.
Bw Putin ameratibiwa kuwa mwenyeji wa viongozi wa Afrika mwezi Juni katika mkutano wa kilele kati ya Urusi na Afrika – wa pili wa aina yake.
Pia unaweza kusoma: