
Mtu mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi huku polisi wakikabiliana na waandamanaji katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
Maelfu ya watu wameitikia wito wa maandamano ya kitaifa ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga, ambaye anadai kuwa uchaguzi uliopita wa Kenya uliibiwa.
Bw Odinga, ambaye amewania urais mara tano, pia anashutumu serikali kwa kukosa kuwasaidia Wakenya kukabiliana na hali ya “kupanda” kwa gharama ya maisha.
Barabara zinazoelekea kwenye majengo muhimu ya serikali katika mji mkuu zimefungwa na makazi rasmi ya rais kufungwa
Baadhi ya matukio makali yamekuwa katika makazi ya Kibera jijini Nairobi – mtaa wa mabanda wenye historia kubwa ya kuunga mkono upinzani.
BBC ilishuhudia waandamanaji wakiweka vizuizi barabarani na kuwarushia polisi mawe. Watu kadhaa wamekamatwa.
“Tulikuja hapa kwa amani, lakini waliturusia vitoa machozi,” Charles Oduor mwenye umri wa miaka 21 aliambia shirika la habari la AFP katika wilaya nyingine ya Nairobi.
“Wanatudanganya kila siku. Uko wapi unga wa mahindi wa bei nafuu wawalioahidi? Ajira walizoahidi vijana ziko wapi? Wanachofanya ni kuajiri marafiki zao.”
Polisi wa kutuliza ghasia pia wamekabiliana na waandamanaji katika mji wa magharibi wa Kisumu, ambapo Bw Odinga anavutia wafuasi washupavu.
Kanda zilizosambazwa na gazeti la Standard la Kenya mapema Jumatatu zinaonekana kuonyesha wahudumu wa magari ya umma wakikimbia vituo vyao vya usafiri katikati mwa Nairobi.
Taarifa za hivi punde kuhusu maandamano ya Kenya na Afrika Kusini
Wakati huohuo, chama cha upinzani nchini Afrika Kusini, Economic Freedom Fighters (EFF), pia kimeandaa maandamano dhidi ya serikali, kumtaka rais aachie ngazi kutokana na kuzorota kwa uchumi, kukatwa kwa umeme na kuenea kwa rushwa.
Maandamano kama hayo yamepangwa nchini Senegal na Tunisia, yakiashiria kuongezeka kwa kutoridhika na marais waliopo madarakani.(BBC Swahili)