Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt. Wilson Charles amewaagiza wasimamizi wa Uchaguzi ngazi ya majimbo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria ili kuepuka malalamiko yanayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Dkt. Charles ametoa agizo hilo wakati anafungua mafunzo ya uchaguzi kwa wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo Kanda ya Ruvuma yenye Mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Iringa na Mbeya, mafunzo hayo yamefanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
“Kama unavyoona Taifa letu sasa hivi kuna baadhi ya watu wanachokochoko sana,kwa hiyo mjitahidi kufanya kazi kwa kanuni na sheria za uchaguzi ili kuepuka shari ya watu hao’’ Dkt. Charles
Amesema hadi sasa NEC imeshatuma sehemu kubwa ya vifaa vya kufanikisha uchaguzi Mkuu ambao unatarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu na kwamba vifaa hivyo vimekwishaanza kusambazwa na inatarajiwa hadi kufikia Oktoba 24 kila Halmashauri nchini itakuwa imepokea vifaa vyote vya uchaguzi.
Amewashauri wasimamizi wa Uchaguzi katika majimbo kuanza kuvipakua vifaa hivyo na kuvisambaza katika maeneo yote na kwamba wasisubiri hadi Oktoba 27.
“NEC katika uchaguzi wa mwaka huu tunataka kuwa tofauti ukilinganisha na mwaka 2015, kwanza Serikali imetuletea fedha zilizotokana na kodi za walipa kodi kwa wakati, hivi tunavyoongea zaidi ya shilingi bilioni 120 nimezishusha ngazi ya Halmashauri’’ Dkt. Charles